Wahusika wa ugaidi wanaswa

Marion Bosire
2 Min Read

Wakili maarufu wa Mombasa Andrew Chacha Mwita, ni mmoja wa watu 22 waliokamatwa kwenye msako uliolenga wanaounga mkono, kufadhili na kufaidi kutokana na ugaidi katika maeneo ya Nairobi, Mombasa, Kapseret, Moyale na Marsabit.

Mwita alitiwa mbaroni Ijumaa Novemba 14, 2025 huko Mombasa kwenye msako wa maafisa wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi ATPU kwa kile kinachosemekana kuwa hatua yake ya kufadhili ugaidi.

Wengine waliokamatwa kwenye msako huo wanaaminika kuwezesha ugaidi, itikadi kali, usajili na ufadhili wa shughuli za kigaidi.

Alifikishwa katika mahakama ya Kahawa ambapo maafisa wa upelelezi waliomba kukubaliwa kuendelea kumzuilia kwa siku 20 zaidi na uamuzi kuhusu ombi hilo utatolewa kesho Novemba 19, 2025.

Kikao cha mahakama cha kusikiliza ombi sawia kwa washukiwa Richard Muriuki Murimi, Said Galgalo Duba, Ali Mohamed na Dhalha Abdi Mohamed waliokamatwa jijini Nairobi kiliandaliwa leo Novemba 18, 2025.

Anthony Odhiambo Odwuor aliyepatikana huko Kapseret naye atafahamu hatima yake Novemba 25, 2025 wakati mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la kuendelea kumzui kwa siku 15 zaidi.

Novemba 26, 2025 mahakama itaamua kuhusu ombi jingine la kuendelea kuzuiliwa kwa siku 20 kwa washukiwa Miriam Ali Abdalla na Aisha Abdullahi waliokamatwa katika kaunti ya Mombasa.

Siku hiyo hiyo washukiwa waliokamatwa huko Marsabit ambao ni Fatuma Yabalo Guyo, Jilo Arafti Halake, Ajirena Halake Sora, Safia Ture Bidu, Kabale Duba Ali na Abdisalam Hassan Charfi watafahamu pia iwapo watazuiliwa kwa siku 30 zaidi.

Share This Article