Wizara ya afya imetangaza kuajiriwa kwa wahudumu wa afya chini ya mpango wa utoaji huduma za afya kwa wote UHC, baada ya ukaguzi uliotekelezwa kote nchini.
Katika taarifa waziri wa Afya Aden Duale alisisitiza kujitolea kwa serikali kuimarisha nguvu kazi katika sekta ya afya ambayo ni nguzo kuu katika kuafikia mpango wa huduma za afya kwa wote na utoaji huduma bora kote nchini.
Mpango wa uhakiki wa wahudumu hao wa afya uliotekelezwa kwa pamoja na idara ya huduma za afya na baraza la magavana ulilenga wahudumu 7,629.
Wahudumu 215 hata hivyo hawakujitokeza kuhakikiwa na wakatajwa kuwa wafanyakazi hewa au wasiohitimu. Mishahara yao imesimamishwa huku uchunguzi ukiendelea.
Waliopatikana kuwa sawa wamegawanywa katika makundi mawili, la wanaoendelea kuhudumu na la wanaokabiliwa na kesi za kinidhamu.
Waziri Duale alielezea kwamba walio kwenye kundi la kwanza watajumuishwa kwenye mfumo wa afya kuanzia mwezi Septemba mwaka huu wa 2025.
Waliosalia watasubiri uchunguzi kuhusu kesi zao za nidhamu kabla ya kufahamu hatima yao kulingana na kanuni za tume ya utumishi wa umma.
Wizara ya Afya inasisitiza kwamba mpango huu unadhihirisha kujitolea kwake kwa uwajibikaji, matumizi faafu ya raslimali na mabadiliko yanayoendelea kwa lengo la kuafikia mpango wa afya kwa wote UHC.