Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajiwa leo Jumatano, Agosti 27, 2025, kufanya zoezi la uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wagombea wa Ubunge na Udiwani kote nchini.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi na masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi huo utaanza saa 1:30 asubuhi na kukamilika saa 10:00 jioni.
Zoezi la uteuzi wa wagombea wa urais litafanyika katika ofisi za INEC, Njedengwa jijini Dodoma, wakati wagombea wa ubunge watawasilisha fomu kwa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo na wagombea udiwani kwa wasimamizi wasaidizi katika ngazi ya kata.
Mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi, INEC imesema majina ya wagombea wote yatabandikwa kwenye mbao za matangazo katika maeneo husika kwa ajili ya ukaguzi wa umma.
Tume imewataka vyama vya siasa na wagombea kuhakikisha wanazingatia muda uliopangwa na maelekezo waliyopatiwa, ili kuepuka changamoto katika zoezi hilo muhimu.