Ilikuwa shangwe,mbwembwe,nderemo na vifijo katika uchanjaa wa kimataifa wa Nelson Mandela Namboole, wakati wenyeji Uganda Cranes, waliwaparamia tembo kutoka Guinea, na kuwachabanga mabao 3-0 katika mechi ya kombe la CHAN ya kundi C iliyopigwa jana usiku.
Waganda waliokuwa wamenyukwa kwa idadi sawa na Algeria, katika mechi ya ufunguzi walianza mechi kwa makeke wakishambulia mara kwa mara na wakachukua uongozi katika dakika ya 29, kupitia kwa Reagan Mpande.
Allan Okello aliongeza la pili kupitia penati kablaya nguvu mpya Ivan Ahimbisibwe alipowakwepa mabeki wa Guinea.
Uganda Cranes iliafiki msemo wa ;ukitaka kula nguruwe chagua aliyenona ,kwani ushindi dhidi ya Guinea umeashiria uwezo wao wa kufuzu kwa hatua ya nane bora.

Ushindi huo umeweka hai matumaini ya Uganda kutinga kwota fainali kwa mara ya kwanza, wakishikilia nafasi ya pili kwa alama 3 ,moja nyuma ya Algeria wakati Guinea ikiwa ya tatu kwa pointi tatu pia.
Afrika Kusini waliotoka sare ya 1-1 na Algeria wamo katika nafasi ya nne kwa alama 1.