Taasisi za afya 4,760 za serikali, 2,498 za kibinafsi, 1,442 za kidini, 17 za jamii na zingine 86 kote nchini zimesajiliwa katika halmashauri ya afya ya jamii SHA.
Katika mkutano wa kila wiki na wanahabari leo Jumatatu, msemaji wa serikali Isaac Mwaura, alisema serikali pia imeshirikisha hospitali 55 za matibabu ya saratani kuwahudumia wakenya katika maeneo mbali mbali kote nchini.
“Serikali pia imeshirikiana na vituo 184 kutoa matibabu ya figo kwa wagonjwa,’ alisema Mwaura.
Kulingana na Mwaura, serikali ilitenga shilingi bilioni tisa kwa halmashauri ya afya ya jamii SHA, kulipa madeni yaliyodaiwa hazina ya bima ya afya NHIF, kabla ya kuanza kutekelezwa kwa SHA.
“Ufadhili huu unajumuisha shilingi bilioni moja kwa mpango ulioimarishwa wa Linda Mama,” aliongeza Mwaura.
Aidha msemaji huyo wa serikali alisema wafanyakazi 20,000 zaidi wamesajiliwa katika bima hiyo ya afya ya jamii.
Kuhusu ukuaji wa uchumi, Mwaura alisema mfumko wa bei umepungua katika sekta muhimu za taifa hili hususan katika sekta za nishati na kilimo.
“Mfumko wa bei umepungua hadi asilimia 3.6, kiwango cha chini zaidi tangu mwaka 2012, kutoka asilimia 9 mapema mwaka huu,” alisema Mwaura.
Alisema kuimarika kwa uchumi, kumesababisha mashirika kadhaa ya serikali yaliyokuwa nakinakili hasara, kuanza kupata faida.