Waendesha baiskeli 12 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DR Congo wameendesha baisikeli kilomita 6,000 wakihamasisha jamii za Afrika Mashariki kuhusu umoja wao na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kundi hilo kwa jina “Great Africa Cycling Safari” linahamasisha jamii kuhusu kuwepo kwa vyakula vya kutosha Afrika Mashariki kwa kupanda miti ya matunda katika maeneo kame, vijijini na shuleni.
Katika safari yao iliyoanza Agosti Mosi nchini Uganda, wameweza kutembelea nchi za Rwanda, Burindi, Tanzania na sasa Kenya kwa kutumia baiskeli zenye bendera za mataifa hayo na sasa wanatoa wito kwa Marais wa Afrika Mashariki kukubaliana kutokuwepo kwa mautumizi ya stakabadhi kwenye mipaka ili kurahisisha utangamano zaidi.
Kulingana John Baptist, kiongozi wa kundi hilo aliyezungumza katika shule ya upili ya Machakos walipopanda miti wakiwa safarini, mbadiliko ya tabia nchi ni janga ambalo linahitaji hatua za dharura na ndiposa wakaanza hamasa ya upanzi wa miti ya matunda katika shule za Afrika Mashariki na vijiji ili kukahikisha kila wakati kuna vyakula vya kutosha.
Kwa mujibu wa Julius Mwenda, mwendesha baiskeli kutoka Kenya, utangamano wa Afrika Mashariki utaimarika zaidi kwa kuwepo uhuru wa kuvuka mipaka ya mataifa hayo bila vizuizi vya stakabadhi.
Kundi hilo likijumuisha mwendesha baiskeli asiyeona kwa jina Antony Mukwanja ambaye anatoa wito kwa walemavu kujitokeza na kuwa na mchango kwenye jamii ya kisasa hususan kukabili madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Hatima ya safari hiyo itakuwa nchini Uganda watakapokamilisha kilomita 6,000 kwa kutumia baiskeli wiki ijayo.