Wadau wa juhudi za kujenga amani kutoka kaunti za Isiolo, Garissa na Mandera wametoa wito kwa serikali zao za kaunti kuhakikisha kuwa zinatenga rasilimali za kifedha ili kuziba pengo lililoachwa na wafadhili, kufuatia uamuzi wa serikali ya Marekani kupitia shirika la USAID kusitisha ufadhili wao kwa miradi ya amani na mshikamano katika maeneo hayo.
Wakizungumza mjini Isiolo baada ya kumalizika kwa warsha ya siku mbili ya kubadilishana uzoefu baina ya kaunti hizo tatu, wadau hao kutoka serikalini na mashirika ya kijamii walitathmini mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na changamoto za pamoja kama vile ulanguzi wa binadamu, misimamo mikali na msimamo mkali wa kidini unaoelekezwa kwenye ugaidi.
Walisisitiza haja ya serikali za kaunti kuhakikisha kuwa juhudi za amani na mshikamano zinaendelezwa bila kusita ili mafanikio yaliyopatikana yasipotee.
Waziri wa Fedha, Mipango ya Kiuchumi, Mshikamano na Utatuzi wa Migogoro wa kaunti ya Isiolo, Luqman Ahmed, alisema kuwa changamoto kuu kwa sasa katika juhudi za kuendeleza amani ni ukosefu wa fedha, kufuatia kujiondoa kwa USAID ambalo lilikuwa mfadhili mkuu wa mashirika mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za mshikamano na ukuzaji wa amani.
Alibainisha kuwa huu ndio wakati mwafaka kwa serikali za kaunti kuingilia kati kuhakikisha kuwa miradi ya ujenzi wa amani inaendelea. Aliongeza kuwa Idara ya Mshikamano na Ukuzaji wa Amani katika kaunti ya Isiolo tayari imepokea maagizo mahsusi kutoka kwa Gavana Abdi Guyo kuongeza juhudi katika shughuli za ukuzaji wa amani ili kuhakikisha kuwepo kwa ushirikiano wa amani baina ya jamii mbalimbali, kufuatia misukosuko ya kisiasa iliyoshuhudiwa hivi karibuni baada ya jaribio la kumbandua Gavana kupitia hoja ya kumwondoa madarakani.
Mohamed Amin, afisa wa mipango katika shirika la Regional Pastoralist Peace Link, alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazokumba kaunti hizo ni pamoja na ulanguzi wa binadamu na msimamo mkali unaoathiri vijana, ambapo wengi wao huvutwa na makundi haramu kutoka nchi jirani ya Somalia. Hata hivyo, alieleza kuwa ukosefu wa fedha unahatarisha juhudi za serikali na mashirika ya kijamii katika kukabiliana na changamoto hizo kupitia mikakati ya kuelimisha na kushirikisha jamii moja kwa moja.
Mkurugenzi wa Mshikamano wa Jamii na Utatuzi wa Migogoro katika Kaunti ya Mandera, Abdirizack Mukhtar, pamoja na Msimamizi wa Kaunti Ndogo ya Garissa Township, Shai Ambe, ambao waliongoza ujumbe kutoka kaunti zao, walipongeza hatua ya kuitisha mkutano huo wa kubadilishana uzoefu baina ya kaunti, wakisema kuwa mkutano huo uliwapa fursa ya kujifunza mbinu na mafunzo muhimu kutoka kwa wenzao wa kaunti jirani.
Kauli hizo ziliungwa mkono na Mwenyekiti wa Mtandao wa Kidini wa Isiolo, Sheikh Ahmed Set, ambaye alisisitiza kuwa suala la usalama, mshikamano na vita dhidi ya matatizo ya kijamii kama misimamo mikali linahitaji ushirikiano wa pamoja kutoka kwa Wakenya wote. Alizitaka serikali zote mbili, ya kitaifa na za kaunti, kuhakikisha kuwa zinatenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya amani, ili kulinda mafanikio yaliyopatikana dhidi ya hatari ya kuyeyuka kutokana na ukosefu wa ufadhili kutoka kwa wafadhili wa nje.