Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amewapongeza wadau katika sekta ya majani chai, kwa mchango wao wa kupigiwa mfano katika ukuaji na maendeleo ya sekta hiyo hapa nchini.
Akizungumza alipofungua rasmi kongamano la Majani Chai la mwaka 2024 katika kaunti ya Mombasa, Dkt. Ronoh alitambua wajibu muhimu unaotekelezwa na wadau wa sekta ya Majani Chai, kwa kuhakikisha taifa hili lina Majani Chai yanayokuzwa hapa nchini ni ya ubora wa hali juu.
“Katika mfumo wa uchumi wa Bottom Up Economic, tunatambua na kuheshimu kiwanda bora zaidi cha Majani Chai, wakulima wetu na wawekezaji ambao wanapiga jeki uchumi wa taifa letu,” alisema Dkt. Ronoh.
Katibu huyo alitoa wito kwa washikadau kukumbatia teknolojia za kisasa za uongezaji dhamani, ili kuifanya Majani Chai ya Kenya kuwa bora zaidi duniani.
Kongamano la Majani Chai la mwaka 2024, lililopewa kauli mbiu “Miaka 100 ya kuhudumia majani chai ya Kenya katika nchi zingine za Ulimwemgu”, ulileta pamoja wadau katika sekta ndogo ya Majani Chai hapa nchini na nje ya nchi, kujadili biashara ya Majani Chai na fursa zilizopo za uwekezaji hapa nchini.