Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amewatahadharisha wanasiasa dhidi ya kutilia shaka utenda kazi Tume Huru mpya ya Uchaguzi na Mpaka (IEBC) kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Mudavadi amesema tume hiyo itafanya uchaguzi huru, wa haki na kuaminika ambapo Rais William Ruto atashinda muhula wa pili kupitia kwenye debe.
“Hebu tukome kutilia shaka uadilifu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). IEBC ni tume huru na itafanya uchaguzi huru na wa haki. Inawakilisha Jamhuri ya Kenya na siyo chombo cha mrengo wowote wa kisiasa,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

Amewaonya wale wanaoeneza uongo kuwa uchaguzi ujao utaibwa ili kumnufaisha Rais Ruto.
Mudavadi aliyasema hayo magharibi mwa nchi wakati wa mkutano wa mipango ya kuwawezesha wanawake na vijana katika maeneo ya Malava na Shinyalu katika kaunti ya Kakamega na kisha katika kaunti ya Busia.
“Hatuko kwenye biashara ya kuiba kura. Ni siasa za pesa nane kuwaambia Wakenya kwamba Ruto ataiba kura. Tuko katika biashara ya kumwambia kila Mkenya kutupigia kura yake. Rais Ruto atashnda kihalali na tuko na imani kwamba atapata muhula wa pili kwa njia rahisi,” aliongeza Mudavadi ambaye uongozi wake umekosolewa na baadhi ya wanasiasa wa eneo la magharibi.

“Mimi nataka kuwaambia wale wanasiasa wa upinzani na pia wale wanaongea wakiwa mrengo wetu wa Kenya Kwanza, wanaosema eti kura ya Rais Ruto itaibwa ama Rais Ruto ataiba kura. Wache nikuzungumza upuuzi. Nataka niwaambie mchana tumsaidie Rais Ruto aingie awamu yake ya pili mwaka 2027. Kisha akishaingia mnitafute mimi Musalia Mudavadi niwaambie ni nini napanga na mwelekeo baada ya 2027 ni upi?”