Wabunge siku ya Jumanne, waliunga mkono uteuzi wa Makamishna wapya wa Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi (NPSC), wakisisitiza haja ya dharura ya kuleta mageuzi katika huduma hiyo huku uhusiano kati ya polisi na umma ukiendelea kuzorota.
Wakiongozwa na mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma, wabunge hao walitoa wito wa kuungwa mkono kikamilifu kwa walioteuliwa, wakidokeza kuwa uteuzi huo unajiri wakati ambapo baadhi ya maafisa wa Huduma ya Taifa ya polisi wamelaumiwa kwa utepetevu.
“Mheshimiwa Spika, kuna changamoto hapa ambayo inahitaji sisi kutafakari jinsi ambavyo tutafurahia uhuru wetu bila kipimo,” alisema Kaluma.
“Maafisa ambao ni wakatili, wanapaswa kuchukuliwa hatua kuambatana na sheria,” aliongeza mbunge huyo.
Aidha alisema Makamishna hao wapya, ni sharti wazingatie haki na usawa.
Kwa upande wake mbunge wa Kajiado Kaskazini Onesmus Ngogoyo pia alitoa wito wa kuwa na mbinu mpya na zinazoleta mageuzi kwenye tume hiyo.
“Tunatazamia kuwa na watu wenye mawazo mapya ambao hawatafuata nyayo za watangulizi wao, lakini watabadilisha tume hiyo,” aisema Ngogoyo.