Wabunge wataka ufafanuzi kuhusu gharama ya miradi ya sekta ya ICT

Wabunge walihoji gharama ya miradi kama Studio Mashinani, vituo vya kidijitali na mtandao wa Wi-Fi wa umma.

Marion Bosire
2 Min Read

Wabunge ambao ni wanachama wa Kamati ya mawasiliano, habari na ubunifu wametaka ufafanuzi wa kina kuhusu gharama ya miradi mbali mbali, deta iliyokusanywa na Worldcoin na malimbikizi ya madeni katika wizara ya habari, mawasiliano na uchumi dijitali.

Viongozi hao walitoa tahadhari kuhusu ukosefu wa uwiano kwenye bajeti na utekelezaji hafifu wa miradi katika sekta ya TEHAMA, kufuatia kikao cha uhakiki na wizara hiyo ya habari, mawasiliano na uchumi dijitali.

Wabunge walihoji gharama ya miradi kama Studio Mashinani, vituo vya kidijitali na mtandao wa Wi-Fi wa umma.

“Mmezindua studio 10 za mashinani kwa miaka 10, sasa mnapangia mbili tu. Mkakati uko wapi?” alihoji Erastus Kivasu. Pia walitaka bajeti za kina, wakieleza tofauti kubwa za gharama na matumizi duni ya fedha.

Madai ya deni ya jumla la bilioni 7.3 pia yalizingatiwa kwa ukali, ambapo wabunge walitaka wizara kulinganisha takwimu zake na zile za wizara ya fedha.

“Ni nani anasema ukweli?” aliuliza naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Alfah Miruka.

Kulikuwa na wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa utekelezaji wa vituo 1,400 vya kidijitali na kutotolewa kwa taarifa wazi kuhusu ufutiliaji wa data iliyokusanywa na Worldcoin.

“Mtafanyaje kuthibitisha kwamba data imefutwa kweli” aliuliza John Kiarie.

Kamati hiyo ilikosoa pia ukosefu wa mshikamano katika usalama wa mtandaoni, miunganisho hafifu katika vituo vya afya na upungufu wa ufadhili kwa mradi wa Chuo Kikuu cha KAIST.

Wakiwa katika mchakato wa kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, wabunge walisisitiza haja ya mkakati ulio wazi, wenye ufanisi na uwajibikaji.

“Hatuwezi kupitisha tu bajeti bila kuchunguza,” alihitimisha Kiarie.

Share This Article