Wabunge wataka kuharakishwa kwa kesi kortini

Jaji Fatuma Sichale alisema kuwa idara ya mahakama inapanga kuongeza majopo 15 ili kuharakisha mchakato wa kusikilizwa kwa kesi hizo.

Dismas Otuke
1 Min Read

Wabunge wametaka kuharakishwa kwa kesi zilizo mahakamani kama mojawapo wa njia ya kuhakikisha usawa, uwazi na haki kwa walalamishi na walioshtakiwa.

Mapendekezo hayo yalitolewa wakati wa kikao cha pamoja kilichoandaliwa jana Alhamisi kati ya Tume ya Huduma za Mahakama – JSC na kamati ya bunge kuhusu utekelezaji wa katiba – CIOC.

Wakizungumza wakati wa kikao hicho, wabunge wa kamati hiyo Geofrey Mulanya na Charles Nguna walihoji kucheleweshwa kutolewa kwa hukumu ya kesi nyingi zilizo mahakamani.

Jaji Fatuma Sichale, aliyekuwa aliyewakilisha JSC, alifichua kuwa kuna mrundiko wa kesi 257,000, zilizo mahakamani zikisubiri kuamuliwa, kukiwa na jopo la majaji tisa pekee wa mahakama ya rufaa wanaopaswa kuzisikiliza.

Aliongeza kuwa idara ya mahakama inapanga kuongeza majopo 15 ili kuharakisha mchakato wa kusikilizwa kwa kesi hizo.

TAGGED:
Share This Article