Wabunge wapitisha Mswada unaojumuisha hazina ya NG-CDF kwa katiba

Tom Mathinji
2 Min Read
Kikao cha Bunge la Taifa.

Bunge la Taifa limepitisha kwa kauli moja mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2025, unaonuia kujumuisha kwenye katiba hazina ya serikali ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge NG-CDF, hazina ya serikali ya kitaifa inayotengewa makundi maalum, NGAAF na hazina ya usimamizi ya Senate, SOF.

Wakati mswada huo uliposomwa kwa mara ya pili bungeni, wabunge  304 walipiga kura kuunga mkono huku hakuna yeyote aliyeipinga. Wakati iliposomwa mara ya tatu, wabunge waliunga mkono mswada huo.

Mswada huo uliowasilishwa bungeni kwa pamoja na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na  Samuel Chepkonga wa Ainabkoi Machi 12,2025, ulipelekewa kwa kamati ya Haki na Maswala ya Katiba ili kufanyiwa ukarabati.

Kamati hiyo ilikusanya maoni ya umma katika maeneo bunge yote 290 na kuwasilisha ripoti yake Juni 17,2025, ikidokeza kuwa asilimia 98 ya waliotoa maoni, waliunga mkono hazina hiyo.

Hazina ya NG-CDF inanuiwa kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma za serikali ya kitaifa hasa elimu na muundomsingi katika kiwango cha mashinani.

Kwa upande mwingine, hazina ya SOF  inalenga kuimarisha jukumu la usimamizi la Senate kwa serikali za kaunti huku ile ya NGAAF ikiimarisha ufadhili kwa maundi yasiyojiweza wakiwemo wanawake, vijana na wale walio na ulemavu.

Kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah aliisifu hazina ya NG-CDF akisema ina manufaa mengi zaidi katika kiwango cha jamii akisema kuwa inajaliza rasilmali za serikali za kaunti.

Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, alizungumzia uhusiano wa mswada huo na katiba akisema kuwa marekebisho hayo yanatofautisha baina ya ugatuzi na kugawa majukumu na unanuia kujaliza ustawi wenye usawa kuambatana na katiba.

Share This Article