Spika wa Bunge la Taifa,Moses Wetang’ula leo Jumatano ameongoza wabunge katika kumwomboleza mbunge wa Malava Moses Malulu Injendi aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Hadi kifo chake, marehemu Injendi alikuwa amehudumu kwa vipindi vitatu bungeni.
Mwenda zake alifariki juzi Jumatatu jioni wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.
Akizungumza alipowaongoza wabunge kuitembelea na kuifariji familia ya marehemu katika makazi yake mtaani South C, Nairobi, Wetang’ula alimtaja Injendi kama kiongozi mwadilifu na mweneza umoja, aliyekuwa na mchango mkubwa katika uundaji wa sera za bunge.
“Malulu Injendi alikuwa miongoni mwa wabunge wanaoheshimika zaidi, akijulikana kwa nidhamu yake, kujitolea kwake kwa mijadala ya bunge, na kazi yake ya kamati. Kama Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, alishiriki pakubwa katika kutengeneza sera zilizoliletea taifa letu manufaa,” aliungama Wetang’ula.

Maoni sawia yalitolewa na wabunge walioandamana naye, wote hao wakimtaja marehemu kama kiongozi asiye na ubinafsi na aliyechapa kazi bila kuchoka kuinua maisha ya wakazi wa Malava.
“Alikuwa mpatanishi, kiongozi aliyekuwa na uwezo wa kuunganisha watu kupitia hotuba zake zenye hekima. Katika kipindi changu kama Spika, sijawahi kusikia Malulu Injendi akiwa na ugomvi na mbunge yeyote,” Wetang’ula aliongeza.
Bunge limeahidi kutoa msaada kamili kwa familia ya marehemu wanapojiandaa kwa mazishi yake.
Mazishi ya Injendi yamepangwa kufanywa Machi 4 mwaka huu katika eneo bunge la Malava, kaunti ya Kakamega.