Wabunge zaidi ya 40 kutoka eneo la Mlima Kenya wametoa wito wa uchunguzi madhubuti kufanywa kuhusiana vurugu na machafuko yaliyosababisha vifo, kujeruhiwa kwa waandamanaji na kuharibiwa kwa mali ya mamilioni ya pesa hasa katika eneo hilo wakati wa maandamano ya Juni 25 na Julai 7 yaliyoshuhudiwa nchini.
Wakiwahutubia wanahabari mjini Naivasha, wabunge hao wanaoegemea serikali ya Kenya Kwanza, wamehusisha yote yaliyotokea na uchochezi uliofanywa na watu wenye maslahi ya kisiasa.
“Tunatoa wito wa kufanywa kwa uchunguzi madhubuti wa machafuko yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Wale waliohusika moja kwa moja kwenye vurugu hizo wanapaswa kukamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria,” walisema wabunge hao kwenye taarifa iliyosomwa na mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie.
“Pia wafadhili na wachochezi wa vurugu hizi wanapaswa kufichuliwa na kuwajibishwa.”
Wameongeza kuwa Kenya ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa na utawala wa sheria na yeyote aliyehusika katika vurugu hizo anapaswa kuchukuliwa hatua kali bila kujali cheo chake katika jamii.
Serikali ya Kenya Kwanza imeulaumu upinzani kwa kuchochea maandamano yaliyosababisha madhara makubwa nchini, madai ambayo upinzani umeyapuuzilia mbali ukiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.