Wabunge wa Azimio watishia kumng’atua Wetang’ula

Hii ni baada ya Spika kubatilisha uamuzi wa mahakama kuu kwamba muungano wao ndio ulio na wabunge wengi.

Marion Bosire
1 Min Read
Spika wa Bunge la taifa Moses Wetangula.

Wabunge wa Bunge la Taifa ambao ni wanachama wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, sasa wanatishia kuwasilisha hoja ya kumng’atua Spika Moses Wetang’ula.

Hii ni baada ya Wetang’ula kubatilisha uamuzi wa mahakama kwamba chama cha Azimio ndicho kilicho na wabunge wengi katika bunge hilo.

Wabunge hao wa Azimio waliondoka bungeni kwa vishindo baada ya uamuzi huo na kuhutubia wanahabari.

Wakiongozwa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed, wabunge hao walitangaza kwamba wameondoa wanachama wao kwenye kamati muhimu ya kuratibu shughuli za bunge.

Hatua hiyo ni ya kulalamikia uamuzi wa Wetang’ula huku Junet akikosoa usemi wa Spika hasa uwepo wa wanachama 14 ambao si wanachama wa Kenya Kwanza au mrengo wa Azimio miongoni mwa shutuma nyingine.

Akitoa uamuzi wake, Wetang’ula alitofautiana na uamuzi wa mahakama kuu na akatangaza kwamba muungano wa Kenya Kwanza ndio una wabunge wengi, uamuzi ambao mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo anasema hawakubaliani nao.

Share This Article