Wabunge wa Azimio kufanya kikao Jumatano

Kikao hicho kimeitishwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Marion Bosire
1 Min Read
Kalonzo Musyoka akihutubu katika kanisa Katoliki

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameitisha kikao cha wabunge wote waliochaguliwa kupitia vyama vya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Jumatano wiki hii.

Musyoka ambaye pia ni mmoja wa viongozi wakuu wa muungano huo amechukua hatua hiyo kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu wa Ijumaa.

Mahakama hiyo ilifutilia mbali uamuzi wa Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetangula la kutangaza Kenya Kwanza kuwa chama cha wengi bungeni.

Kalonzo alifichua kwamba tayari amewasiliana na Raila Odinga na Uhuru Kenyatta kuwajuza kuhusu mkutano huo wa wabunge wa Azimio, muungano uliotajwa na mahakama kuu kuwa chama kilicho na wabunge wengi bungeni.

Akihutubia hafla moja ya mazishi huko Kitui, Kalonzo alisema kwamba uamuzi huo wa mahakama ni funzo kwa viongozi waliokuwa kwenye muungano wa Azimio kabla ya kuhamia Kenya Kwanza, akishangaa kuhusu imani yao katika muungano huo.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ambao ni John Chigiti, Lawrence Mugambi na Jairus Ngaah liliamua kwamba Spika Wetang’ula angefuata sheria alipotangaza Kenya Kwanza kuwa chama cha wengi bungeni.

Awali, Kalonzo alikuwa ameelekeza wabunge wa Azimio wakalie viti vya walio wengi bungeni na kutwaa nyadhifa za wengi bungeni vile vile.

Share This Article