Viwanja vya Bukhungu na Kanduyi kukamilishwa kwa wakati

Waziri wa michezo Salim Mvurya na Gavana wa Kakamega Fernandez Barasa walizuru uwanja wa Bukhungu.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Michezo Salim Mvurya na Gavana wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa, wamewahakikishia wakazi na wananchi kwa jumla kwamba viwanja vya Bukhungu na Kanduyi kaunti jirani ya Bungoma vitakuwa tayari kwa maandilizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, ambayo Kenya inatarajiwa kuwa mwenyeji.

Wakizungumza baada ya kukagua ujenzi wa awamu ya pili wa uga wa Bukhungu, viongozi hao walielezea kuridhishwa kwao na maendeleo ya mradi, wakiahidi wenyeji kuwa viwanja hivyo vitakuwa vimekamilika kwa maandalizi ya mashindano hayo.

Serikali kuu ilichukua usimamizi wa ukarabati wa uwanja huo katikati ya mwaka 2024 ili kuharakisha kukamilishwa kwake kabla ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Awali, mradi huu ulikwama kwa madai ya ukosoefu wa fedha katika ngazi ya kaunti na mvua kubwa.

Alipozuru uwanja huo mapema mwaka huu, Rais William Ruto alitoa amri kwamba kazi hiyo ikamilike kufikia katikati ya mwaka 2026 ili kuzingatia viwango vya kimataifa.

Mbali na Bukhungu, Waziri Mvurya pia amesema wanalenga kumaliza  uwanja wa Masinde Muliro ulioko Kanduyi, Kaunti ya Bungoma akisema kwa sasa umefikia kiwango cha asilimia 90.

Share This Article