Kama njia ya kuzitia mshawasha timu za Kenya, Uganda na Tanzania kufanya vyema katika makala ya nane ya kombe la CHAN, viongozi wa nchi hizo zinazoandaa kipute hicho wametoa ahadi si haba ya pesa kwa timu zao endapo zitanyakua kombe.
Rais wa Kenya William Ruto alitoa ahadi ya shilingi milioni 600 kwa Harambee Stars endapo watanyakua kombe hilo hilo la CHAN wakishiriki kwa mara ya kwanza kama wenyeji.
Aidha, Ruto aliahidi kutuza kila mchezaji wa Harambee Stars shilingi milioni moja kwa kila ushindi na nusu milioni kwa kila sare.
Upande wa pili wa sarafu Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa ahadi ya kuituza Taifa Stars shilingi milioni 51 za Kenya endapo watanyakua kobe la CHAN.
Rais Yoweri Kaguta Museveni pia aliahidi shilingi milioni 43 kwa kila ushindi.
Mapema Jumatatu Rais Ruto ametimiza ahadi yake ya shilingi milioni 28, au milioni moja kwa kila mchezaji na maafisa watatu wa benchi ya kiufundi baada ya kusajili ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya DR Congo Jumapili.
Kocha wa Kenya Benni McCarthy akizungumza kwenye mahojiano baaa ya mechi alikiri kuwa uwepo wa Rais Ruto uwanjani na kuzungumza na wachezaji kabla ya mechi na wakati mapumziko kuliwatia motisha wachezaji.
Endapo vishawishi hivyo vitazisukuma timu za Afrika Mashariki kufika nusu fainali na mojawapo kunyakua kombe ni jambo la kubainika kadri ya kipute kinapoendelea.