Visa vya Mpox vyathibitishwa Nyandarua na Laikipia

Tom Mathinji
4 Min Read

Hali ya wasiwasi imekumba baadhi ya maeneo ya kaunti za Laikipia na Nyandarua, kufuatia kuthibitishwa kwa visa vya ugonjwa wa Mpox (zamani ikijulikana kama Monkey pox).

Watu watatu wamegunduliwa kuugua ugonjwa huo katika Kaunti ya Nyandarua, huku mmoja akibainika kuwa na ugonjwa huo kwenye Kaunti ya Laikipia.

Maafisa wa afya wamethibitisha kuwa kesi mbili za kwanza zinawahusu wanandoa kutoka kijiji cha Maili Nne, eneo bunge la Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua.

Wanandoa hao  Elkanah Kibet mwenye umri wa miaka 25 na mkewe Ruth Mwihaki mwenye umri wa miaka 23, waligunduliwa kuwa na Mpox baada ya kuonyesha dalili kama vile homa, kutetemeka kwa mwili, vidonda vyenye maumivu kwenye ngozi, na maumivu makali kwenye sehemu za siri.

Wanandoa hao walikuwa wametoka safari ya hivi majuzi mjini Mombasa na walitafuta matibabu katika Kituo cha Afya cha Baari kilichoko Maili Nne kabla ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyahururu, ambako sasa wanapokea matibabu maalum.

Watoto wawili wenye umri wa miaka mitatu na miezi mitatu waliokuwa karibu na wagonjwa hao, wako chini ya uangalizi wa kitabibu.

Hadi sasa, watoto hao hawajaonyesha dalili zozote, lakini bado wanazidi kufuatiliwa kwa tahadhari.

Mwathiriwa wa tatu aligunduliwa katika eneo la Kinangop, Kaunti ya Nyandarua, na kufikisha  idadi jumla ya maambukizi katika kaunti hiyo kufikia tatu.

Maafisa wa afya wanasema mgonjwa huyo ametengwa na tayari amepokea huduma za matibabu.

Maafisa wa afya katika kaunti za Laikipia na Nyandarua, kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, wameanzisha juhudi za ufuatiliaji wa watu waliotangamana na wagonjwa na kampeni za uchunguzi ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Laikipia, Dkt. Albert Wagura Taiti, aliwahakikishia wakazi kuwa hatua zote muhimu za kudhibiti maambukizi zimechukuliwa.

“Tunachukulia hali hii kwa uzito mkubwa. Tumeanzisha michakato muhimu ya kutenga wagonjwa na kudhibiti maambukizi, na tunashirikiana kwa karibu na Wizara ya afya kufuatilia hali hii. Mpox ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa iwapo utagunduliwa mapema. Tunawahimiza wananchi wote wenye vipele visivyoeleweka, homa, au maumivu ya mwili kutafuta matibabu mara moja,” alisema Dkt. Taiti.

Mwenzake wa Kaunti ya Nyandarua, Juliana Syoweu Tsinanga, pia alitoa kauli kama hiyo akisema kuwa kikosi cha pamoja cha uchunguzi na uhamasishaji tayari kiko mashinani kikifanya kazi.

“Tumehamasisha vikosi vyetu vya dharura na tunafanya kazi kwa pamoja na Kaunti ya Laikipia kuhakikisha kuwa maambukizi hayaendelei. Tunawaomba wakazi wabaki watulivu lakini waripoti dalili zozote haraka iwezekanavyo,” alisema Bi. Tsinanga.

Akizungumza kwa njia ya simu, Gavana wa Nyandarua, Dkt. Kiarie Moses Badilisha, aliwataka wakazi kutokuwa na hofu.

“Wahudumu wetu wa afya wako katika hali ya tahadhari, na tayari tumewatambua watu wote waliokaribiana na familia iliyokuwa safarini Mombasa. Hakuna haja ya hofu kwani hali iko chini ya udhibiti,” alisema Gavana Badilisha.

Mpox ni ugonjwa wa virusi unaoambukizwa kutoka kwa mtu aliyeambukizwa, wanyama, au vifaa vilivyochafuliwa. Ingawa si mara zote huua, unaweza kusababisha madhara makubwa hasa kwa watoto na watu wenye kinga dhaifu ya mwili.

Timu za afya ya umma katika kaunti zote mbili zimeanza kampeni za uhamasishaji katika jamii huku wahudumu wa afya wakivalia mavazi ya kujikinga. Wananchi wanahimizwa kudumisha usafi wa hali ya juu, kuepuka kushikana ovyo, na kuripoti haraka visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya Mpox.

Ingawa hali bado inadhibitiwa, mamlaka hazijafunga milango kwa uwezekano wa kubainika kwa kesi zaidi huku shughuli za ufuatiliaji na upimaji zikiendelea.

Share This Article