Viongozi wa kaunti ya Kiambu wameonya kuhusu ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia huku kaunti hiyo ikiongoza kwa idadi ya visa viliyoripotiwa nchini.
Mbunge wa Thika Mjini, Alice Ng’ang’a, amesema kuwa angalau wanawake 46 wameuawa katika visa vinavyoshukiwa vya mauaji ya wanawake huho Thika pekee mwaka huu.
Akizungumza kwenye kongamano la wanawake mjini Thika, Ng’ang’a aliwataka wanandoa kudumisha uaminifu, akitaja usaliti kuwa chanzo cha migogoro ya nyumbani na mauaji.
“Usaliti unavunja familia na kugharimu maisha,” alionya mbung huyo.
Mshiriki wa kongamano hilo, Miriam Wayua, alihimiza jamii kuripoti visa vinavyoshukiwa na kuomba serikali kuimarisha mpango wa nyumba kumi ili kufichua visa vinavyojificha vijijini.
Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kiambu, Anne Wamuratha, alisema hali ya kaunti ya Kiambu kuwa na mchanganyiko wa watu kutoka maeneo mbalimbali inachangia ongezeko la visa hivyo na kufichua kuwa viongozi wamezungumza na Rais william Ruto kuhusu kupata msaada wa kitaifa kukabiliana na janga hilo.
Mbunge wa Gatundu Kaskazini, Elijah Njoroge, naye alitaja usaliti kwa kueneza migogoro na mauaji ya nyumbani na kuwataka wanandoa kuwa waaminifu na wawazi ili kuepusha migongano.
Viongozi hao waliahidi kuendelea kushinikiza utekelezaji mkali wa sheria, uhamasishaji wa jamii na huduma za msaada ili kukomesha ukatili wa kijinsia na kulinda wanawake na wasichana katika kaunti ya Kiambu.