Viongozi wataka wahusika wakuu wa mauaji ya Charles Were wachukuliwe hatua

Tom Mathinji
3 Min Read
Viongozi watoa wito wa kukamatwa kwa wahusika wa mauaji ya mbunge Charles Ong’ondo Were.

Viongozi  wa mirengo yote ya kisiasa, wametoa wito kwa asasi za usalama kuharakisha kuwakamata waliohusika katika mauaji ya mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were.

kulingana na viongozi hao, wale ambao wamekamatwa na maafisa wa polisi, walitumika tu lakini waliofadhili kifedha mauaji hayo bado wako mbioni

Wakizungumza wakati wa mazishi ya mbunge huyo katika shule ya msingi ya Karabok, kaunti ya Homa Bay, viongozi hao walisema familia ya mbunge huyo na wakazi wa eneo bunge la Kasipul watapata haki pale wahusika wakuu watakapokamatwa.

Wakiongozwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, viongozi hao walikashifu maujai hayo wakiyataja kuwa mauaji ya kisiasa ambayo yanapaswa kutokomezwa hapa nchini.

“Tunalaani vikali mauaji ya mbunge Charles Were. Tunatoa wito kwa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI na afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma, kuharakisha kesi hiyo na kuhakikisha wale waote walihusika wanchukuliwa hatua,” alisema Wetang’ula.

Akizungumza katika mazishi hayo, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, pia alitaka kesi hiyo iharakishwe, akidokeza kuwa wale ambao wako mahakamani ni mawakala tu lakini wahusika wakuu bado hawajakamatwa.

“Tunapopongeza kazi ya maafisa wa polisi, sisi kama chama cha ODM tunasema kuwa wale ambao wamekamatwa ni mawakala tu. Tunataka wahusika wakuu wa mauaji haya wamatwe mara moja,” alisema Raila.

Raila alionya kuwa wale ambao wanamharibia sifa Were kupitia mitandao ya kijamii, wanaweza husishwa na mauaji yake.

Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi John Mbadi, aliunga mkono matamshi ya kutaka wahusika wakuu wa mauaji hayo kutiwa nguvuni.

Gavana wa Migori Dkt. Ochillo Ayacko alishtumu wale wanaomharibia sifa mbunge huyo kupitia mitandao ya kijamii, akisema ni pigo maradufu kwa familia ya Were ambayo inaomboleza.

Kwa upande wake, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliwahimiza maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wahusika wakuu wanatiwa mbaroni.

“Tunawaeleza polisi kwamba, licha ya kwamba mmewakamata mlinzi na dereva wa mbunge huyo pamoja na kupata silaha iliyotumika, ni wakati sasa wa kuwakamata wahusika wakuu,” alisema Sifuna.

Matamshi sawia na hayo yalitolewa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge Seneta Johnson Muthama, mbunge wa Kipkelion Magharibi Hillary Kosgei na mbunge wa Homa Bay mjini  Peter Kaluma.

Share This Article