Rais William Ruto ameonya viongozi wa kidini na wa kisiasa dhidi ya kuchochea vijana kutekeleza maandamano na kusababisha vurugu akisema kwamba watachukuliwa hatua.
Alikuwa akizungumza jana katika shule ya upili ya Simotwo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet wakati wa uzinduzi wa awamu ya tisa ya mpango wa kila mwaka wa utunzaji mazingira na uboreshaji maisha.
Kiongozi wa nchi alionya kuhusu athari mbaya watakazokumbana nazo wale wanaozua Fujo, machafuko na uharibifu wa mali.
Alitaja mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi na uvamizi wa vituo vya polisi kuwa vitendo vya kigaidi ambavyo ameapa kuvishughulikia ipasavyo.
Rais Ruto alisema taifa limeshuhudia machafuko ya hali ya juu katika muda wa miezi michache iliyopita, machafuko anayosema yanafadhiliwa na viongozi wachache wenye nia mbaya.
Ruto aliwakashifu viongozi wa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa kukosa mpango makhsusi kwa taifa hili akiwataka waangazie kuunganisha nchi na kushughulikia masuala makuu yanayoathiri taifa.
Alidhihirisha ujasiri kwamba atawashinda wanasiasa wa upinzani kwa kiwango kikubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 na kupata muhula wa pili uongozini kutokana na maendeleo aliyoleta na ahadi alizotimizia wakenya.
Rais Ruto alitaja miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, uboreshaji wa mfumo wa huduma za afya na mpango wa kazi majuu kuwa sehemu ya ile aliyotekelezea wakenya.
Alisema pia kwamba utawala wake umeimarisha uchumi na kupunguza mfumko wa bei za bidhaa muhimu.