Baadhi ya viongozi wanawake katika kaunti ya Mombasa wametoa wito kwa Rais William Ruto kutoa kipaumbele kwa uimarishaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika eneo hilo, wakielezea mashaka juu uungwaji mkono wa chama hicho mashinani na kukosa kutambuliwa kwa wanachama waaminifu.
Wakiongozwa na mratibu wa rais katika kaunti ya Mombasa Mildred Odinga, wanawake hao wamemtaka Ruto kuongeza jitihada zaidi kuelekea kuimarisha msingi wa chama hicho, badala ya kutegemea muungano jumuishi.
“Tunaunga mkono serikali jumuishi, lakini pia tunahitaji kuimarisha chama chetu,” alisema Odinga wakati wa mkutano na wanahabari mjini Mombasa.
“Wale waliosimama kidete na Rais na chama cha UDA wakati wa kampeni hawapaswi kutengwa wakati huu ambapo kuna muungano mpya.”
Viongozi hao walielezea kutorodhishwa kwao na usambazaji wa rasilimali za serikali, hasa zille zinazolenga kuwawezesha wanawake katika kaunti hiyo.
Walidai kuwa watu wanaoegemea mirengo pinzani ya kisiasa wanavuna kule ambako hawakupanda badala ya wafuasi wa UDA.
“Wakati Rais anapotuma fedha za kuwawezesha wanawake Mombasa, viongozi wa eneo hili wanaoegemea chama cha ODM wanazisambaza kwa watu wao,” alidai Odinga.
“Mwenendo huu unawavunja moyo wafuasi waaminifu wa UDA wanaohisi kutengwa.”
Taarifa ya KNA