Viongozi mbali mbali nchini wakiongozwa na Rais William Ruto, wametoa jumbe za kumwomboleza mbunge na waziri wa zamani Dalmas Otieno ambaye aliaga dunia jana Jumapili asubuhi.
Katika ujumbe wake wa rambi rambi, Rais Ruto alimsifia Otieno ambaye alikuwa mbunge wa zamani wa eneo la Rongo kwa kuwa mwanasiasa mwenye maono na msimamo.
Waziri aliye na mamlaka makuu na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi alimtaja marehemu Otieno kama mtumishi wa umma aliyejitolea na ambaye nidhamu na uadilifu wake umeacha urithi wa kudumu.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alimkumbuka Otieno kama mtu mtulivu na mwenye kuunganisha watu aliyeheshimiwa na mirengo yote ya kisiasa kutokana na ustadi na uongozi wake wenye msimamo dhabiti.
Kwa upande wake, Waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen alimtaja Otieno kuwa mwanateknolojia mashuhuri ambaye atakumbukwa kwa mbinu yake ya kupima maswala mbalimbali kwenye uzani, uhuru wa kimawazo na kujitolea kwake katika utumishi wa umma.
Naibu Mkuu wa Wafanyakazi, Eliud Owalo alisema Otieno alikuwa kiongozi mahiri, mtulivu, mlumbi stadi, mwenye maono, na mfanyabiashara stadi na mwenye shauku isiyoyumba ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Otieno atakumbukwa pia kwa kushinikiza kuongezwa kwa umri wa kustaafu kutoka miaka 55 hadi 60 hali iliyosaidia wengi na kwa juhudi za kusaidia wasiojiweza katika jamii.