Viongozi wa Mlima Kenya washauriwa waepuke siasa za ubinafsi waige umoja wa Magharibi

Marion Bosire
3 Min Read
Mwangi Kiunjuri - Mbunge wa Laikipia Mashariki

Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, amewasihi viongozi wa eneo la Mlima Kenya waache kushiriki katika matusi na siasa za kugawanya watu, na badala yake wazingatie kushughulikia masuala yanayowaathiri moja kwa moja wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla mbili za kuchangisha fedha katika Kaunti ya Nyandarua, Kiunjuri alisisitiza umuhimu wa umoja na uongozi unaolenga maendeleo. Aliwasifu wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya kwa uwezo wao wa kuweka kando tofauti za kisiasa kwa ajili ya maendeleo ya pamoja, na kuwataka viongozi wa Mlima Kenya kuiga mfano huo.

“Tuige viongozi kutoka Magharibi mwa Kenya ambao licha ya tofauti zao za kisiasa, huungana kwa ajili ya maendeleo ya eneo lao. Ni lazima tuache siasa za ubinafsi zinazowanufaisha watu wachache na tuangalie maslahi ya wananchi,” alisema Kiunjuri.

Akiwa ameandamana na Mbunge wa Laikipia Magharibi, Wachira Karani, na Mbunge wa Ol Kalou, David Kiaraho, Kiunjuri aliwataka wakazi wa Nyandarua kutoingia katika siasa kwa hasira na kukata tamaa. Alitoa wito wa uvumilivu, akieleza kuwa serikali inahitaji muda kutekeleza ahadi zake.

Wabunge hao watatu waliongoza harambee katika wadi za Rurii na Kaimbaga katika eneobunge la Ol Kalou, ambapo walichangisha fedha kusaidia vikundi vya wenyeji. Katika mikutano hiyo, wakazi walieleza kutoridhishwa kwao na jinsi serikali inavyoshughulikia masuala muhimu kama Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), ucheleweshaji wa malipo ya wazee, na miundombinu duni ya barabara.

Kiunjuri alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na akaeleza jitihada za serikali katika kuzitatua, hasa kuhusu Mfumo wa utathmini wa Mahitaji wa SHA ambao umekosolewa. Alisema kuwa mfumo huo kwa sasa unawawekea wananchi mzigo mkubwa wa kifedha na akasisitiza kuwa marekebisho yanahitajika ili kuhakikisha unakuwa wa bei nafuu.

Kwa upande wake, Mbunge Kiaraho alitetea uungwaji wake mkono kwa serikali, akisema kuwa serikali inaleta mafanikio halisi ya maendeleo katika eneobunge lake, ikiwemo uboreshaji wa barabara na miradi ya umeme vijijini.

Viongozi hao walitoa wito wa kuachana na malumbano ya kisiasa na kuhimiza uongozi wa huduma unaozingatia maslahi ya wananchi, huku wakitaka wanasiasa na wananchi kwa ujumla washiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wa eneo hilo.

Share This Article