Viongozi kaunti ya Meru, wamelaani vikali ghasia na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya Saba Saba, wakitaja matukio hayo kuwa uhalifu wa kiuchumi ambao haupaswi kutokea tena.
Kwenye mkutano na wanahabari jana,kamishna wa kaunti ya Meru Jacob Ouma, gavana Isack Mutuma,pamoja na wazee wa Njuri Ncheke wakiongozwa na Adriano Aruyaru walielezea hisia zao kuhusiana na uharibifu mkubwa wa biashara na mali ya umma.Gavana Mutuma alionya kwamba ghasia hizo zililemazwa pakubwa shughuli katika sehemu hiyo.
Aliwahimiza wakazi na viongozi kushirikiana na kuzingatia amani.
Kamishna wa kaunti ya Meru Jacob Ouma,alithibitisha kwamba washukiwa 103 walitiwa mbaroni na maafisa wanatumia picha za CCTV kuwatambua washukiwa zaidi wa ghasia hizo.
Wafanyibiashara huko Meru kupitia mwenyekiti wao Jacob Muungania waliwahimiza wakazi kulinda mali yao huku wakitoa wito kwa polisi kuimarisha usalama.
Aliwaonya wanasiasa dhidi ya kufadhili visa vya ghasia na uharibifu.Wakati huo huo, msemaji wa Njuri Ncheke Adriano Aruyaru alitoa wito kwa wazazi kuwa washauri wa watoto wao hasa wale wa kizazi cha Gen Z kuhusu athari za kujihusisha na uhalifu.