Viongozi wa kike kutoka sehemu mbali mbali za nchi walikongamana leo katika hoteli ya Safari Park kwa mkutano ambao kauli mbiu yake ilikuwa ‘Inuka na Ujenge Upya kwa Imani na Neema Thabiti”.
Mkutano huo unajiri kabla ya mkutano wa 22 wa maombi ya kitaifa wa kiamsha kinywa utakaoandaliwa kesho asubuhi na ulihudhuriwa na viongozi wa kike katika sekta mbali mbali kama siasa, dini na hata uanaharakati.
Lengo lake lilikuwa kuangazia uponyaji wa kitaifa na jukumu la pamoja.
Mkutano wa leo uliandaliwa na chama cha wabunge wa kike ambao ni wakristo na ulisisitiza jukumu muhimu la wanawake katika ujenzi wa taifa kupitia maombi, umoja na uongozi stadi.
Wenyeviti wenza wa chama hicho Naomi Waqo na Veronica Maina walishauri wanawake wakumbatie wito wao wa kipekee wa kukuza amani, upendo na mafanikio.
“Tumeona kile ambacho Mungu anaweza kutenda wakati wanawake wanaomba,” alisema Seneta Maina akiongeza kwamba mambo sio kama kawaida tena na kuna haja ya kuinuka, kujenga upya na kuongoza kwa neema.
Mnenaji mkuu katika mkutano huo Mtume Isi Igenegba kutoka Nigeria alitaka viongozi wabadili mawazo akisisitiza haja ya kujitolea na maamuzi ya kijasiri yatakayobadili taifa.
Waziri Alice Wahome alikariri wito wa umoja hata baada ya siasa akiwahimiza wanawake washirikiane katika kushughulikia mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya wakenya.
Huku Rais William Ruto akitarajiwa kuhudhuria maombi ya kesho, mkutano wa leo umeweka mandhari ya uwezeshaji yanayoongozwa na wanawake wa imani waliojitolea kuunda Kenya bora.