Viongozi wa kidini watoa wito wa ukomavu wa kisiasa nchini

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi wa kidini wakiwahutubia wanahabari

Kongamano la Pamoja la Mashirika ya Kidini la Ufungamano limetoa wito kwa serikali ya Kenya Kwanza kudumisha katiba, kuheshimu haki za raia na kuiondoa nchi kutoka kile lilichokitaja kuwa janga la kitaifa linalonukia.   

Wakiwahutubia wanahabari leo Alhamisi, wanachama wa kongamano hilo, linalowaleta pamoja wawakilishi kutoka Kanisa Baptisi la Kenya, Kanisa la Friends (Quakers), Kanisa la Kiprotestanti na Shirila la Ufuatiliaji wa Haki za Binadamu nchini Kenya, walitoa wito wa ukomavu wa kisiasa, uwajibikaji na usitishaji mara moja wa ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji.

Viongozi hao wa kidini walisisitiza kuwa Kenya inakaribia kukabiliwa na uharibifu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa, wakionya kuwa semi za hivi karibuni za kisiasa na utumiaji wa nguvu kupita kiasi unaofanywa na asasi za serikali vinatishia kuisambaratisha nchi hii.

“Umuhimu wa bunge na serikali kuu kuwa na ukomavu wa kisiasa ni wa dharura zaidi kwa wakati huu kuliko wakati wowote ule,” viongozi hao walisema kwenye taarifa yao.

Walitoa wito kwa viongozi kuheshimu sauti za watu kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 1 cha Katiba ambacho kinakabidhi Wakenya mamlaka makuu.

Wakitoa mfano wa maandamano yenye vurugu ya Juni 25 na Julai 7  almaarufu Saba Saba, kongamano hilo lililaani vifo, kujeruhiwa kwa waandamanaji na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa wakati wa maandamano hayo na kuwatuhumu polisi kwa kusababisha vyote hivyo.

“Kwa kuwaamrisha polisi kufyatua risasi hadi kuua, wanaamriwa kuharibu hekalu la Mungu anakoishi Roho Mtakatifu,” walionya viongozi hao.

Matamshi yao yanakuja siku moja baada ya baadhi ya viongozi wa kidini kukutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi jana Jumatano.

Wakati wa mkutano huo, viongozi hao waliwataka Wakenya kumpa Rais Ruto muda wa kutosha kuitumikia nchi na kuunga mkono jitihada za kiongozi wa nchi kujenga kanisa katika Ikulu.

Taarifa ya Victor Kiplagat na Yvone Wanjiru wa KNA

 

Share This Article