Viongozi wa Kenya Kwanza wausuta upinzani kwa kueneza siasa za kikabila

Martin Mwanje
2 Min Read
Prof. Kithure Kindiki - Naibu Rais

Viongozi wa utawala wa Kenya Kwanza leo Ijumaa walipeleka injili ya utawala huo katika kaunti ya Trans Nzoia walikoipigia debe serikali ya Rais William Ruto wakisema imefanya mengi kwa kipindi kifupi ambacho imekuwa madarakani kuboresha maisha ya Wakenya. 

Kaunti ya Trans Nzoia ni ngome ya kisiasa ya Gavana George Natembeya, mkosoaji mkubwa wa utawala wa Kenya Kwanza na ambaye anaegemea mrengo wa upinzani.

Kwenye ziara yao, Naibu Rais  Prof. Kithure Kindiki aliwaongoza viongozi wa Kenya Kwanza kuusuta upinzani wakiulaumu kwa kuchochea maandamano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini katika siku za hivi karibuni.

Hususan, waliunyoshea upinzani kidole cha lawama kwa kueneza siasa za chuki na kuigawanya nchi, ukiongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na Gavana Natembeya.

Akizungumza katika uwanja wa shule ya upili ya wavulana ya Kipkekei katika eneo bunge la Cherangany wakati wa hafla ya kuchangisha fedha za kuwawezesha wanawake iliyoratibiwa na Mwakilishi wa Wanawake wa Trans Nzoia  Lilian Siyoi, Prof. Kindiki alisema serikali ya Kenya Kwanza ina rekodi bayana ya maendeleo inayoweza ikakaguliwa.

Naibu Rais alisikitika kuwa upinzani hauna suluhu mbadala kwa matatizo yanayoikumba nchi lakini unatumia nafasi yake kuwachochea na kuwagawanya Wakenya.

Kulingana naye, serikali ya Kenya Kwanza imejibidiisha kubadilisha maisha ya Wakenya na kuhakikisha maendeleo yanatekelezwa kwa usawa kote nchini.

Aiyasema hayo wakati upinzani ukiendelea kuushutumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kufanya maisha kuwa magumu zaidi kwa Wakenya wengi.

Unatoa mfano wa kodi nyingi wanazotozwa Wakenya, ikiwemo kodi ya nyumba na Mamlaka ya Afya ya Jami, SHA, kodi ambazo unataka serikali kufutilia mbali.

Upinzani umeapa kuhakikisha unamwondoa Rais Ruto madarakani wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Kwa upande wake, Rais Ruto ameuonya upinzani dhidi ya kutumia njia za mkato kutaka kuingia madarakani.

Share This Article