Viongozi wa dini wapaza sauti kuhusu utekaji nyara

Askofu mkuu wa kanisa la kianglikana nchini Jackson Ole Sapit, anataka maelezo ya wanaotekeleza utekaji nyara yawekwe wazi.

Marion Bosire
2 Min Read

Askofu mkuu wa kanisa la kianglikana nchini Jackson Ole Sapit anataka serikali ielezee wakenya kuhusu watu ambao wanatekeleza utekaji nyara wa vijana na mauaji ya baadhi yao.

Akizungumza jana katika kanisa la St. Philips huko Kisii, Ole Sapit alisema serikali ina wajibu wa kuhakikishia raia wake ulinzi na usalama.

Kiongozi huyo wa dini anataka huduma ya taifa ya polisi NPS nayo iwajibike kwa kufahamisha wakenya kuhusu wanaolenga vijana katika uovu huo.

Alionya dhidi ya balagha ya kikabila inayoenezwa na viongozi wa kisiasa katika sehemu mbali mbali za nchi pamoja na uhamasihaji wa kikabila ambao anasema umeunganishwa na vitosho na huenda ukahatarisha mshikamano wa kitaifa.

Wakati huo huo viongozi wa dini kutoka kaunti ya Migori wamelaumu viongozi wa kisiasa kwa kujaribu kuficha utendakazi wao duni kupitia visa vinavyoshuhudiwa vya utekaji nyara.

Wakiongozwa na askofu John Okinda wa kanisa la PEFA, viongozi hao wa dini walidhihirisha wasiwasi kwamba utekaji nyara unatumiwa kuondoa fikra za wakenya kutoka kwa hatua ya serikali kukosa kutekeleza majukumu yake.

Askofu Okinda alisema maisha ni matakatifu na wanasiasa hawafai kuendesha masuala kama hayo wapendavyo ili kujiendeleza kisiasa.

Maoni ya Okinda yalikaririwa na askofu John Adawo, aliyesisitiza kwamba ni lazima viongozi watimize ahadi walizotoa wakati wa kampeni kwani wakenya wako macho.

Share This Article