Viongozi mbalimbali wamwomboleza Wafula Chebukati

Chebukati alifariki jana Alhamisi jioni wakati akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi. Alikuwa na umri wa miaka 63. Alihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC kati ya mwaka 2017 na 2023.

Martin Mwanje
3 Min Read
Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kuzikwa nyumbani kwake Trans Nzoia.

Rais William Ruto aliwaongoza viongozi mbalimbali nchini kuomboleza kifo cha Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati. 

Chebukati alifariki jana Alhamisi jioni wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.

Hadi kifo chake, alikuwa na umri wa miaka 63.

“Nimepokea taarifa za kufariki kwa Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati kwa huzuni mkubwa,” alisema Rais Ruto kwenye risala yake ya rambirambi.

“Chebukati alikuwa kiongozi mwenye msimamo na mwerevu aliyetumikia taifa kwa uadilifu. Kifo chake ni pigo kwa nchi yetu.”

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta pia amesikitishwa na kifo cha Chebukati, akisema kwa kipindi alichohudumu, alitekeleza wajibu muhimu katika kuleta mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi wa nchi.

“Naifariji familia yake, marafiki, na wafanyakazi wenzake wakati huu mgumu wa maombolezo,” alisema Uhuru.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula katika risala yake alimlimbikizia sifa Chebukati amkimtaja kuwa mtu aliyefanya kazi zake kwa uadilifu.

“Kama mwanasheria mwenye sifa tele, Chebukati alikuwa mfano wa heshima na uadilifu wa taaluma ya sheria,” alisema Wetang’ula.

“Wakati akihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC, alitekeleza majukumu yake kwa ujasiri wa hali ya juu, kwa kutii katiba, na dhamira isiyoyumba kwa haki. Hata wakati wa changamoto, alisalia kuwa imara, akiongozwa na kiapo chake cha utendakazi na kanuni za usawa na uwazi.”

Matamshi sawia yalitolewa na Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi ambaye binafsi anaomboleza kifo cha baba yake.

“Chebukati alisimamia chaguzi zenye usawa na uwazi ambazo zimeendelea kuhamasisha utawala wa sheria na maongozi nchini Kenya,” alisema Kingi kwenye ujumbe wake wa maombolezo.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, kwa upande wake, alimtaja marehemu kuwa mtu mwenye hekima.

“Daima nitamkumbuka kama mtu imara na mwenye busara, aliyekabiliana na nyakati ngumu kwa ujasiri, haki na dhamira isiyoyumba ya uwazi. Mchango wake kwa maongozi ya uchaguzi utasalia himizo la kudumu kwa wale wanaopigania haki na uongozi bora,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi pia alimwomboleza Chebukati akimtaja kuwa mtu aliyeheshimu misingi ya demokrasia.

“Muhula wa Wafula Chebukati kama Mwenyekiti wa IEBC ulitawaliwa na kujitolea na dhamira thabiti kwa kanuni za demokrasia. Uongozi wake katika kusimamia mchakato wa uchaguzi ulitekeleza wajibu muhimu katika kubadilisha maongozi ya nchi,” alisema Waziri Muturi.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka pia ameelezea kuhuzunishwa kutokana na kifo cha Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya IEBC.

“Natuma risala za rambirambi kwa familia na marafiki wa Mwenyekiti wa zamani wa IEBC Wafula Chebukati,” alisema Kalonzo katika ujumbe mfupi.

 

 

Share This Article