Baadhi ya viongozi wa kaunti ya Laikipia wamepinga kutolewa kwa ekari 300 za ardhi ya umma kwa Dorcas Rigathi ambaye ni mke wa Naibu Rais wa zamani, Rigathi Gachagua.
Ardhi hiyo, iliyoko Kandutura karibu na mji wa Rumuruti, ilitolewa kwa Dorcas Gachagua kwa ajili ya kujenga kituo cha kuwasaidia waathiriwa wa matumizi ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, hatua hiyo imezua ghadhabu miongoni mwa viongozi wa eneo hilo ambao wanasema kuwa ardhi hiyo kubwa ingetumika kuwasaidia wakazi wasio na ardhi.
Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia, Jane Kagiri, pamoja na mbunge wa Laikipia Kaskazini, Sarah Korere, waliongoza madai ya kufutiliwa mbali kwa ugawaji huo. Walisema kuwa ni kinyume cha haki kutoa ardhi kubwa namna hiyo kwa watu wa nje huku familia za wenyeji zikiendelea kuishi katika hali duni.
“Kuna makubaliano kati yangu, mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, na Mheshimiwa Korere kwamba hatuwezi kukubali kuendelea kwa ugavi wa ardhi kubwa kwa watu wa nje ilhali watu wetu bado hawana ardhi,” alisema Bi. Kagiri.
Korere alifafanua kuwa hawapingi uanzishwaji wa kituo cha kuwarekebisha waathiriwa wa dawa za kulevya, bali walihoji sababu ya kuhitajika kwa ekari 301 kwa mradi huo.
Alisema kuwa maelfu ya wananchi bado wanateseka katika maeneo kama Kandutura, African Location, Kahari, na Kambi ya Robert.
“Tunaunga mkono wazo la kuwa na kituo cha kuwarekebisha vijana kwa sababu matatizo ya afya ya akili yanayotokana na dawa za kulevya, pombe, na hata uraibu wa mitandao ya kijamii yameathiri sana vijana wetu. Lakini ekari 10 zinatosha kabisa kwa kituo kama hicho,” alisisitiza Korere.
Mwakilishi Wadi ya Sosian, Parletto Lekopien, aliunga mkono matamshi ya viongozi hao, akisema kuwa si watu binafsi tu, bali pia mashirika makubwa yamekuwa yakipewa vipande vikubwa vya ardhi katika kaunti hiyo.
Alitoa wito wa kufutwa kwa utoaji wa ardhi hiyo kwa shirika la Dorcas Rigathi Foundation.
Viongozi hao waliitaka serikali ya kitaifa na mashirika husika ya ardhi kutathmini upya utoaji wa ardhi hiyo na kuhakikisha kuwa rasilimali za ardhi zinawanufaisha wakazi wa eneo hilo, hasa wale wasio na ardhi.