Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), imesema wanajeshi wake wanaokabiliana na makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC ), wataanza kuondoka nchini humo kupitia Rwanda.
SADC ilisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya Rwanda kukubali vikosi hivyo vilivyokuwa vikipambana na waasi mashariki mwa Congo kutumia ardhi yake hadi Tanzania.
Mkuu wa Vikosi Vya SADC nchini DRC Jenerali Rudzani Maphwanya, alisema kundi la wataalam liko nchini Tanzania kutayarisha mipango ya kuondoka kwa wanajeshi hao.
Jeshi la SADC lilipelekwa kuisaidia serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kukabiliana na makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo mwezi Disemba mwaka 2023.
Katikati ya mwezi Machi, Jumuiya ya SADC yenye wanachama 16 ilitangaza kuwa imehitimisha rasmi mamlaka ya kikosi chake cha kijeshi kinachojulikana kama SAMIDRC, na kwamba itaendelea na mchakato wa kuondoa wanajeshi wake kutoka DRC kwa awamu.