Vijana wahimizwa kuwania nafasi za uongozi katika jamii

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga.

Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga, ametoa wito kwa vijana kujitokeza na kuwania nafasi za uongozi katika jamii.

Akizungumza wakati wa hafla ya tatu ya Bunge la Vijana iliyoandaliwa katika Baraza la kaunti ya Kwale siku ya Alhamisi, Chidzuga alidokeza kuwa serikali ya Rais William Ruto imewashirikisha vijana katika mipango kadhaa, ili kuwapiga jeki kujikimu maishani.

Baadhi ya mipango ya serikali aliyoyataja ni pamoja na vituo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano vya Jitume, nafasi za ajira katika miradi mbalimbali ya serikali na hazina ya Hustler.

Naibu Msermaji wa Serikali katika Baraza la Vijana kaunti ya Kwale.

Aidha, Msemaji huyo wa Serikali alisema ili vijana waweze kunawiri maishani, ni sharti watilie maanani nidhamu na maadili.

“Nawataka vijana kuwa na Maadili mema kwani uongozi unaanza na nidhamu katika jamii,” alisema Chidzuga.

Zaidi ya vijana 50 kutoka kaunti sita walihudhuria mkutano huo katika kaunti ya Kwale.

Share This Article