Vijana wahimizwa kukumbatia kilimo cha kisasa

Tom Mathinji
1 Min Read
Mama Taifa Rachel Ruto awahimiza vijana kukumbatia kilimo cha kisasa.

Mama Taifa Rachel Ruto, ametoa wito wa kujumuishwa kwa vijana katika utekelezaji wa mbinu za kisasa za kilimo.

Kulingana na Mama Taifa, utumizi wa ubunifu katika kilimo, unatarajiwa kuongezeka na hivyo kufanikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini.

Aliyaema hayo leo Alhamisi alipofungua rasmi Kituo cha Uvumbuzi wa Kilimo cha Kantaria, katika Chuo Kikuu cha Nairobi bewa la Upper Kabete.

“Kituo hiki kitatekeleza utafiti na uvumbuzi. Wakati mawazo haya yanafunzwa katika taasisi za kiufundi, vituo vya Wizara ya Kilimo na majukwaa ya kijamii, yatawafikia wakulima, shule na soko za karibu,” alisema Mama Taifa.

Mama Taifa alisema kuwa, Rais William Ruto anaamini kuwa, iwapo wakulima watapata pembejeo bora za kilimo, ujuzi na teknolojia, hawatapata tu mazuno ya kumezewa mate, lakini pia watahakikisha mustakabali dhabiti wa taifa hili.

Bi. Ruto alisema sekta ya kilimo ni muhimu sana, kwa kuhakikisha utoshelevu w chakula, huku akidokeza kuwa Kituo cha Uvumbuzi wa Kantaria kitawezesha ongezeko katika uzalishaji wa chakula na shughuli za kibiashara.

Kituo hicho kilichofadhiliwa na kampuni ya Elgon Kenya, kitatumika kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa kilimo.

Share This Article