Vijana wahimizwa kuchukua nafasi za uongozi hapa nchini

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta awasihi vijana kuchukua nafasi za uongozi hapa nchini.

Vijana hapa nchini wamehimizwa kuchukua nafasi za uongozi, huku wakizingatia maadili, unyenyekevu na haki.

Akizungumza wakati wa dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa kwa mahafali wa Kenyatta Trust Jijini Nairobi, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitoa wito kwa vijana kuhakikisha kila wakati wanatekeleza haki na kudumisha amani.

“Ninawahimiza kukumbatia unyenyekevu na kuchukua uongozi. Ongozeni kwa kuzingatia maadili, haki na kila wakati mkiwa na amani moyoni wenu,” alisema Kenyatta.

Uhuru alisema kizazi kijacho lazima kipinge shinikizo za kushiriki ufisadi, migawanyiko au tamaa ya ubinafsi, huku akiwakumbusha wahitimu hao kuwa uongozi sio vyeo bali ni tabia, ujasiri na nia ya kutumikia wengine.

“Tulilenga kuhakikisha tunakuza watu wasio na ukabila au kuegemea upande wowote,” aliongeza Rais huyo mstaafu.

Dhifa hiyo ya chakula cha jioni ilikuwa ya kuwasherehekea wasomi 41 ambao wamekamilisha elimu yao ya shahada ya kwanza na ya juu katika taasisi mbalimbali nchini Kenya na nje ya nchi.

Share This Article