Kundi la vijana wa chama cha ODM limepinga vikali kuteuliwa kwa Harold Kimuge Kipchumba kuwa mbunge mteule wa ODM.
Siku chache zilizopita, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitangaza kuteuliwa kwa Kipchumba kumrithi John Mbadi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
Mbadi alihudumu kama mbunge mteule wa ODM katika Bunge la Taifa kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri.
Wakiongozwa na John Ketora ambaye aliteuliwa na ODM kumrithi Mbadi, vijana hao wanamtuhumu mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon kwa kupuuza matamanio ya chama chao.
Kwenye barua iliyoandikwa na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa chama Edwin Sifuna Julai 24, ODM iliitarifu IEBC kuwa imemteua John Antira Ketora kumrithi Mbadi, wito ambao ulitua kwenye sikio la kufa.
Vijana hao sasa wameapa kuelekea mahakamani kupinga uteuzi wa Kipchumba, wametishia kuigura ODM ikiwa matakwa yao hayatashughulikiwa.