Vijana 700 kunufaika na mpango wa Nyota Isiolo, asema Katibu Liban

Martin Mwanje
2 Min Read
Mohamed Liban - Katibu katika Wizara ya Nishati

Katibu wa Idara ya Petroli katika Wizara ya Nishati, Mohamed Liban, jana Jumatatu  alizindua rasmi mpango wa kuwapatia vijana fursa za kujiendeleza kiuchumi (NYOTA) katika kaunti ya Isiolo, hatua muhimu katika juhudi za kuwawezesha vijana kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Liban alitangaza kuwa vijana 70 watachaguliwa kutoka kila wadi kati ya wadi kumi zilizoko katika kaunti ya Isiolo, na hivyo kufanya jumla ya vijana watakaonufaika na mpango huo kuwa 700.

Alisisitiza kuwa mradi huo umewalanga vijana ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu, kwa lengo la kuwapatia ujuzi na fursa za kujiajiri au kuajiriwa.

“Serikali ina nia ya dhati kuhakikisha hakuna kijana anayeachwa nyuma. Wale ambao hawakufika chuo kikuu bado wana nafasi ya kufanikisha maisha yao, na programu kama NYOTA zimebuniwa kuwainua na kuwajengea matumaini,” alisema Liban.

Kwa wale wanaotaka kujiandikisha katika mpango wa NYOTA, wametakiwa kupiga nambari *254# kwenye simu zao kisha kuchagua chaguo la ‘NYOTA Project’.

Liban alitoa matamshi hayo baada ya kukutana na maafisa wa utawala kutoka sehemu mbalimbali za kaunti ya Isiolo.

Maafisa hao wamepewa jukumu la kuendesha kampeni za uhamasishaji kupitia mikutano ya hadhara maarufu kama baraza, ili kuhakikisha vijana wengi wanajulishwa kuhusu fursa hiyo.

“Huu ni mpango wa kaunti nzima. Tunawategemea machifu wetu na maafisa wa utawala kuwafikia vijana kila kona ya Isiolo na kuwaeleza kuhusu nafasi hii muhimu,” aliongeza.

Mpango wa NYOTA ni sehemu ya mkakati mpana wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi, uongozi, na ujasiriamali.

Uzinduzi huo katika kaunti ya Isiolo unatarajiwa kuchochea harakati za usajili na uteuzi wa kundi la kwanza la wanufaika katika wiki chache zijazo.

Share This Article