Vidosho wa Kenya wanusia WAFCON, baada ya kuwazabua Tunisia

Starlets walifuzu kwa mara ya kwanza kwa kipute cha Afrika mwaka 2016.

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya-Harambee Starlets, inakaribia kufuzu kwa kipute cha kuwania kombe la mataifa ya Afrika (WAFCON) kwa mara ya pili mwaka ujao.

Hii ni baada ya kusajili ushindi wa bao moja kwa bila jana jioni nchini Tunisia, dhidi ya wenyeji katika mkumbo wa pili wa raundi ya kwanza  mechi za kufuzu.

Kenya ilikuwa imeambulia sare tasa katika duru ya kwanza iliyosakatwa Nairobi wiki jana.

Tereza Engesha, alipachika bao pekee na la ushindi kunako dakika ya tatu ya mechi hiyo huku wakiiingia raundi ya pili na ya mwisho ambapo watamenyana na Gambia kati ya tarehe  20 na 28 mwezi Oktoba mwaka huu, kwa mkumbo wa kwanza na wa pili.

Starlets walifuzu kwa mara ya kwanza kwa kipute cha Afrika mwaka 2016.

Timu 11 zitakazoshinda raundi ya mwisho Oktoba mwaka huu zitafuzu kwa dimba la WAFCON nchini Morocco mwaka ujao, zikijumuishwa na wenyeji kuunda idadi ya mataifa 12.

Share This Article