Utekaji nyara: Waziri Muturi ataka tume ya uchunguzi kubuniwa kubaini ukweli

Martin Mwanje
2 Min Read
Justin Muturi - Waziri wa Utumishi wa Umma

Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ametoa wito wa kubuniwa kwa tume ya uchunguzi ili kutegua kitendawili cha ni nani wanaotekeleza visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela nchini na kuwawajibisha wahusika. 

Muturi, ambaye mwanawe alitekwa kabla ya kuachiliwa huru mwaka jana, amesema tume hiyo inapaswa kujumuisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Chama cha Wanasheria nchini, LSK na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini miongoni mwa taasisi zingine.

Amelalamikia kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela aliyosema ni jambo linalozitia hofu familia nyingi na kumtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kukomesha jinamizi hilo.

Wito sawia umetolewa na Seneta wa kaunti ya Makueni Dan Maanzo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Africa Hussein Khalid.

Waziri Muturi aliyazungumza hayo alipofika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nairobi (zamani kikijulikana kama City Mortuary) leo Ijumaa kusimama kidete na familia za wanaume wanne waliotekwa nyara katika eneo la Mlolongo mwezi Disemba mwaka jana.

Mwili wa mmoja wa wanaume hao, Justus Musyimi, ulipatikana katika chumba hicho jana Alhamisi.

Aidha, mwili wa mateka mwingine kwa jina Martin Mwau ulipatikana chumbani hapo.

Hiyo inamaanisha kuwa ni mateka wawili, Kalani Muema na Stephen Kavingo ambao bado hawajulikani waliko, na familia zao zimekita kambi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nairobi kufuatia ripoti kwamba huenda miili ya wapendwa wao nayo ipo chumbani hapo.

Khalid anasema taarifa walizo nazo zinaashiria kuwa miili ya wawili hao ipo chumbani hapo na kwamba ukweli utadhihirika kufikia kesho Jumamosi baada ya kuchukuliwa kwa alama za vidole na vipimo vya vinasaba kufanywa kwani miili hiyo ilikatwakatwa kiasi cha kutoweza kutambulika.

Shutuma dhidi ya visa vya utekaji nyara nchini zimeongezeka katika siku za hivi karibuni huku utawala wa Kenya Kwanza ukitakiwa kuvikomesha kabla ya mambo kwenda mrama.

Na huku polisi wakituhumiwa, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amekanusha madai ya kuhusika kwa maafisa wake katika visa hivyo akiongeza kuwa uchunguzi unaendelea kwa lengo la kuwawajibisha wahusika.

Share This Article