Utambuzi wa taifa la Palestina waghadhibisha Israel

Marion Bosire
4 Min Read
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Hatua ya nchi za Magharibi ya kutambua taifa la Palestina iliibua hasira kubwa nchini Israel jana Jumapili, huku mawaziri wa serikali wakitaka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa uunganishwe rasmi na Israel kama hatua ya kulipiza kisasi.

Uingereza, Canada na Australia zilitambua taifa la Palestina jana Jumapili, hatua inayochukuliwa kuwa msukumo wa kidiplomasia kuelekea suluhisho la mataifa mawili katika mgogoro wa Wapalestina na Waisrael.

Katika taarifa ya video, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema atatoa majibu rasmi kuhusu kutambuliwa kwa taifa la Palestina baada ya kurejea kutoka Marekani.

“Taifa la Kipalestina halitaanzishwa,” Netanyahu alisisitiza, akibainisha kuwa amekuwa akizuia jambo hilo kwa miaka mingi kwa kuimarisha makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi na ataendelea kufanya hivyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilitaja utambuzi huo kuwa “zawadi kwa Hamas ya jihadi.”

Waziri wa Usalama wa Taifa mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, Itamar Ben-Gvir, alitaka serikali ya Israel ichukue hatua za haraka alizozitaja kuwa ni pamoja na kuunganisha Ukingo wa Magharibi na “kuisambaratisha kabisa Mamlaka ya Palestina.”

Kupitia mtandao wa kijamii wa kampuni ya Marekani X, Ben-Gvir alisema atawasilisha pendekezo la kuunganisha Ukingo wa Magharibi katika kikao kijacho cha serikali.

Waziri wa Fedha mwenye msimamo mkali, Bezalel Smotrich, pia alitaka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa uunganishwe kama jibu kwa hatua ya Magharibi kutambua taifa la Palestina.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, huu ndio wakati, na iko mikononi mwako,” Smotrich alisema katika taarifa yake.

Waziri wa Utamaduni na Michezo, Miki Zohar, naye alitoa wito kama huo wa kuunganishwa kwa Ukingo wa Magharibi, akitaja kutambuliwa kwa taifa la Palestina kuwa “tamko lisilo na maana lenye harufu ya chuki dhidi ya Wayahudi na uhasama dhidi ya Israel.”

“Jibu sahihi pekee kwa tamko hili la kijinga ni kutekeleza mamlaka kamili ya Israeli katika Yudea, Samaria (Ukingo wa Magharibi), na Bonde la Yordani,” alisema kwenye X.

Yair Golan, kiongozi wa chama cha upinzani cha Democrats na aliyewahi kuwa Naibu Mkuu wa Jeshi, alitaja kutambuliwa kwa taifa la Palestina kuwa “kushindwa kwa kisiasa kwa Netanyahu na Smotrich – hatua ya uharibifu kwa usalama wa Israel.”

“Hili ni zao la moja kwa moja la kutengwa kisiasa kulikofanywa na Netanyahu: kukataa kumaliza vita na kuchagua kwa makusudi sera hatari ya uvamizi na uunganishaji wa maeneo,” Golan alisema, akitoa wito kwa msimamo wa kisiasa thabiti wa kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.

Kiongozi wa upinzani Yair Lapid alitaja kutambuliwa kwa taifa la Palestina kuwa “janga la kidiplomasia,” akilaumu serikali ya Netanyahu kwa kusababisha “mgogoro wa kidiplomasia mkubwa zaidi kuwahi kutokea.”

Nchi kadhaa nyingine, zikiwemo Ubelgiji, Ufaransa, na Ureno, zinatarajiwa kutambua rasmi taifa la Palestina katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki hii.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni walihitimisha kuwa Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza, ambako zaidi ya watu 65,000 wameuawa tangu Oktoba 2023.

Takriban robo tatu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari zimetambua Palestina, huku Ireland, Uhispania, na Norway zikiwa zimefanya hivyo rasmi mwaka jana.

Share This Article