Utafutaji wa mvuvi aliyetoweka katika shambulizi la Todonyang unaendelea, asema Murkomen

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen akihutubu wakati wa mkutano wa Jukwaa la Usalama, kaunti ya Turkana

Jitihada za kumtafuta na kumwokoa mvuvi wa Kenya aliyeripotiwa kutoweka baada ya kutekelezwa kwa shambulizi la Todonyang, kaunti ya Turkana zinaendelea.

Shambulizi hilo liliripotiwa kutekelezwa na jamii ya Dassanach kutoka nchi jirani ya Ethiopia.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen anasema serikali haiwezi ikaelezea idadi hasa ya vifo vilivyotokana na shambulizi hilo kwa sababu jitihada za kutafuta waliotoweka zinaendelea.

“Kisheria, utaratibu unahitaji kwamba hatima ya waliotoweka hakika iweze kubainika. Baadhi ya ripoti zinaashiria kuwa wale walioripotiwa kufariki wako hai nchini Ethiopia, lakini ukweli ni kwamba, imechukua muda mrefu mno,” alisema Murkomen ambaye awali alihudumu kama Waziri wa Michezo.

Aliongeza kuwa wale walioathiriwa na shambulizi hilo siyo tu jamii ya eneo hilo bali pia wafanyabiashara kutoka maeneo ya Lodwar, Kitale, Kibish, na maeneo mengine.

“Tutaendelea na jitihada za utafutaji na uokozi ili kuwajibikia wale wote walioripotiwa kutoweka. Mchakato huo umeathiriwa na ukosefu wa fedha.”

Waziri Murkomen alikuwa akijibu maswali ya wanahabari baada ya mkutano wa usalama uliofanyika katika eneo la Lodwar leo Jumatano.

Waziri huyo ameanza ziara ya siku tatu katika kaunti za Turkana, West Pokot, na Samburu chini ya mpango wa Jukwaa la Usalama.

Share This Article