Usimamizi wa msanii wa muziki kutoka Nigeria 2Baba umetoa taarifa rasmi, msanii huyo anapotimiza umri wa miaka 50 na miaka 25 katika tasnia ya muziki.
Katika ujumbe huo rasmi shukrani zilitolewa kwa mashabiki, wenzake wa kazi na wafuasi wake kote duniani kwa upendo mkubwa waliomwonyesha.
“Nyinyi ndio moyo wa mafanikio yake na nguzo za urithi wake wa kudumu” ilisema taarifa hiyo.
Kuanzia siku zake za mwanzo akiwa kwenye kundi la Plantashun Boiz hadi kuwa mmoja wa nguli wanaoheshimika zaidi katika muziki wa Afrika, 2Baba amekuwa taa ya matumaini, umoja, na uvumilivu.
Kupitia vibao visivyopitwa na wakati kama African Queen na kazi yenye mchango mkubwa kwa jamii, ameweza kuinua vizazi na kuiwakilisha Afrika kimuziki duniani kote.
“Safari hii si tu kuhusu muziki, bali ni kuhusu urithi” timu yake ilisema, ikiahidi muziki zaidi, tuzo za kimataifa na athari ya kudumu katika miaka ijayo.
Wakati mashabiki barani kote wakijiunga katika sherehe, ujumbe uko wazi, 2Baba hana tu umri wa miaka 50 ya kuvutia yeye ni gwiji.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya ujumbe mwingine sawia ambao 2Baba alichapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akiahidi sherehe ya kipekee kwa mashabiki wake.