Ushirikiano wa kimkakati kati ya Kenya na China kuboresha kilimo

Martin Mwanje
1 Min Read
Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh akiwa na ujumbe kutoka China

Kenya na China zimesisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimkakati unaoangazia biashara, miundombinu na kilimo. 

Hii ilibainika wakati Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh alipotembelewa na ujumbe kutoka China ili kutafuta fursa za uwekezaji kwa kutumia nafasi ya Kenya kama lango la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na uwezo wake unaopanuka wa kibiashara.

Mkutano huo ulisisitiza maono ya Kenya ya kufanya kilimo kuwa cha kisasa na kuhamasisha usalama wa chakula kupitia teknolojia na ubunifu.

Dkt. Ronoh alielezea uwezekano wa ushirikiano katika uzalishaji wa mbolea ya biokaboni, vituo vya uchakataji vya kilimo na suluhu za kidijitali za kilimo.

Aidha, wakati wa mkutano huo, pendekezo liliwaslishwa la kuanzisha kituo cha kutengeneza mashine za kilimo nchini Kenya.

Kituo hicho kitahudumia eneo pana la EAC na kuboresha usafirishaji.

Fursa zingine zilizoangaziwa ni uongezaji wa thamani kwa mimea kama vile kahawa, matunda ya makadamia na maharage ya soya.

Kwa upande mwngine, wawekezaji wa China walipata mwaliko rasmi wa kushiriki Mkutano wa Uwekezaji wa Kilimo wa Kenya uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Share This Article