Ushirikiano kati ya asasi za serikali za usalama na kampuni za walinzi wa kibinafsi, umechangia pakubwa katika kukabiliana na ugaidi pamoja na makundi mengine ya wahalifu hapa nchini.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya kudhibiti kampuni za walinzi wa kibinafsi Fazul Mohamed, ufanisi huo umefanikishwa na kuwepo kwa walinzi wa kibinafsi katika majengo muhimu ya kibiashara na afisi na uwezo wao wa kutangamana kwa urahisi na wananchi.
“Uwepo wa walinzi wa kibinafsi katika vituo vya kibiashara, benki na makazi ya kibinafsi, unapiga jeki juhudi za kuhakikisha usalama unadumishwa na pia rasilimali zinalindwa,” alisema Fazul kupitia taarifa.
Matamshi ya Fazul yanajiri huku taifa hili likiadhimisha miaka kumi tangu kutokea kwa shambulizi la Westgate Jijini Nairobi, ambapo watu 67 walifariki na wengine wengi kujeruhiwa.
Fazul alisema hatua ya serikali ya kushirikiana na walinzi wa kibinafsi, imefanikisha upatikanaji wa habari za kijasusi, utambuzi wa mapema wa visa vya uhalifu pamoja na ukusanyaji na uhifadhi wa ushahidi.
Alipongeza utumizi wa teknolojia katika kukabiliana na changamoto za kiusalama hapa nchini, akisema hatua hiyo itasaidia katika kudhibiti hatari za kiusalama sio tu hapa nchini mbali pia katika kanda hii kwa jumla.
Katika taarifa ya kuadhimisha miaka kumi tangu kutokea kwa shambulizi hilo, Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema nchi ya Kenya inaimarisha uwezo wake taratibu kupitia kuajiriwa kwa maafisa zaidi wa usalama, kuanzishwa kwa vikosi maalum, utoaji wa programu za kisasa za mafunzo kwa maafisa wa usalama na uimarishaji wa uwezo wa kupiga silaha kama inayoelezwa katika Mpango wa Kuwapa Polisi Silaha za Kisasa.
“Lengo letu hatimaye ni kuendeleza uangalizi wa kiwango cha juu kwenye mipaka yetu na operesheni za usalama za kisiri na za wazi kote nchini na kumwangamiza adui kabla ya kutokea kwa mashambulizi,” amesema Dkt. Omollo.