Mahakama ya Rufaa imedumisha ushauri wa Tume ya Uratibu wa Mishahara na Marupurupu (SRC) kuhusu marupurupu ya nyumba kwa wabunge na kiwango cha juu zaidi cha marupurupu ya vikao vya bunge.
Katika uamuzi wake leo Jumatano, mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi lililowasilishwa na Tume ya Huduma za Bunge – PARLSCOM – kupinga mamlaka ya SRC juu ya malipo ya wabunge.
Mvutano ulianza pale ambapo tume ya huduma za bunge ilifanya uamuzi wa kuwalipa wabunge shilingi elfu 250 kama marupurupu ya nyumba na kukataa kuweka kiwango cha juu cha marupurupu ya vikao vya bunge.
Mahakama ilibaini kwamba hatua hizo za tume ya huduma za bunge ni kinyume cha katiba.
Iliamua kwamba PARLSCOM ilikiuka mamlaka yake kwa kuidhinisha marupurupu ya wabunge bila idhini ya SRC.
Mahakama hiyo ya Rufaa kadhalika ilifafanua kwamba SRC haijadhibiti idadi ya vikao vya kamati za bunge bali ilikuwa imeweka kiwango cha juu zaidi cha marupurupu ya vikao ambayo wabunge wanaweza kulipwa.
Kulingana na mahakama, SRC ilifanya hivyo kulingana na mamlaka iliyopatiwa na katiba ya nchi hii ya kudhibiti na kusimamia malipo kwa maafisa wa serikali.
Mahakama hiyo ilisisitiza kwamba matendo ya SRC yanawiana na jukumu lake na mfumo wa kikatiba la kuhakikisha kwamba pesa za umma zinasimamiwa ipasavyo.
Uamuzi huu wa mahakama unathibitisha mamlaka ya kipekee ya SRC ya kuweka viwango vya mishahara na marupurupu kwa maafisa wa serikali na hivyo kulinda uadilifu wa matumizi ya pesa za umma katika kulipa mishahara.