Usalama waimarishwa nje ya mahakama ya Kisutu ambapo Tundu Lissu anatarajiwa

Lissu atawasilishwa mahakamani leo baada ya kususia vikao vya kesi dhidi yake vilivyoendeshwa kwa njia ya mtandao.

Marion Bosire
2 Min Read

Usalama umeimarishwa nje ya mahakama ya hakimu mkazi wa Kisutu ambapo kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu anatarajiwa kuwasilishwa leo Mei 19, 2025.

Mahakama hiyo iliamuru kwamba afikishwe mahakamani moja kwa moja leo baada ya kesi zinazomkabili moja ya uhaini na nyingine ya kueneza habari za uwongo kuendeshwa kwa njia ya mtandao awali.

Lissu alifikishwa kwenye mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 akikabiliwa na mashtaka ya uhaini na uchochezi. Katika shtaka la uhaini, Lissu anadaiwa kudhihirisha nia ya kuchochea umma kususia uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Anadaiwa kutekeleza kosa hilo Aprili 3, 2025 katika mkoa na Dar es salaam.

Lissu anawasilishwa mahakamani leo moja kwa moja baada ya kukataa kuhudhuria vikao vya kesi dhidi yake kwa njia ya mtandao akisema kufikishwa mahakamani ni haki yake.

Haya yanajiri saa chache baada ya kiongozi wa chama cha People’s Liberation cha Kenya Martha Karua ambaye pia ni wakili kufurushwa Tanzania alikokuwa amewasili kwa ajili ya kesi ya leo ya Tundu Lissu.

Karua na mawakili Gloria Kimani na Lynn Ngugi walikuwa wamewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere nchini Tanzania lakini wakazuiliwa humo kabla ya kurejeshwa nchini.

Katibu mkuu wa CHADEMA John Mnyika alilaani hatua ya serikali kumzuia Karua na mawakili wengine wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki kuingia nchini Tanzania kufuatilia kesi ya mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu.

Share This Article