IEBC yazindua zoezi la usajili wa wapiga kura nchini

Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika katika kaunti ya Kajiado na kuhudhuriwa na mwenyekiti na makamishna wa IEBC na Gavana wa Kajiado, Joseph ole Lenku.

Marion Bosire
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini – IEBC leo Jumatatu imezindua zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura, ikitoa fursa nyingine kwa Wakenya wanaostahiki kujisajili kama wapiga kura wapya kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wapiga kura ambao tayari wamesajiliwa kusasisha taarifa zao kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon aliwaongoza makamishna wa tume hiyo katika kuzindua zoezi hilo la kitaifa la usajili wa wapiga kura katika kaunti ya Kajiado.

Hafla ya uzinduzi huo pia ilihudhuriwa na Gavana wa Kajiado Joseph ole Lenku.

Wote hao wakitoa wito kwa Wakenya ambao hawajajisajili kama wapiga kura kutumia fursa hiyo kujiandikisha kama wapiga kura kwani hiyo ndio silaha yao bora katika kuamua mustakabali wa uongozi wa nchi siku zijazo.

Awali, IEBC katika tangazo lake ilisema kuwa zoezi hilo litafanyika katika afisi zote za maeneo bunge nchini, isipokuwa maeneo yanayotarajiwa kufanya chaguzi ndogo.

Kwa mujibu wa tume hiyo, mpango huo ni sehemu ya jukumu lake la kudumisha daftari la wapiga kura lililo na taarifa za hivi punde za wapiga kura na la kuaminika, ambalo ni nguzo muhimu ya mchakato wa uchaguzi ulio wazi na jumuishi.

Huduma zitakazotolewa wakati wa zoezi hilo ni pamoja na usajili mpya wa wapiga kura, urekebishaji au uingizwaji wa taarifa za mpiga kura za hivi punde, uhamisho wa usajili hadi eneo lingine la uchaguzi na uhakiki wa taarifa za mpiga kura.

Huku hayo yakijiri, IEBC inaendeleza mchakato wa kuandaa chaguzi ndogo katika maeneo mbali mbali nchini ambazo zimepangiwa kuandaliwa kwa pamoja Novemba 27, 2025.

Share This Article