Zoezi la kuwasajili makurutu wa polisi wa cheo cha konstebo litaendelea kama ilivyopangwa awali.
Hii ni baada ya kesi iliyokuwa imewasilishwa mahakamani kupinga kufanyika kwa zoezi hilo kuondolewa leo Jumanne.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na kituo cha Sheria Mtaani.
Mawakili wa kituo hicho wamemwambia Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi kwamba wamepokea simu na arafa zaidi ya 20,000 kutoka kwa wazazi wa vijana wanaotaka kujiunga na idara ya polisi wakikiomba kituo hicho kuondoa kesi hiyo.
Aidha, wazazi walitaja idadi kubwa ya maafisa wa polisi watakaohitajika kudumisha usalama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, ikizingatiwa baadhi ya maafisa wametumwa nchini Haiti kusaidia kudumisha usalama nchini humo.
Ni wito ambao kituo hicho kimeridhia kwa kuondoa kesi na hivyo kupisha kuendelea kwa zoezi hilo kama ilivyopangwa.
Naye Jaji Mugambi aliridhia ombi la kuondoa kesi hiyo akisema aliridhika na sababu zilizotolewa.
Hii ina maana kwamba zoezi la kuwasajili makurutu wa polisi litaendelea kama ilivyopangwa kati ya Oktoba 3 na 9.
Makurutu wa polisi wapatao 10,000 wanalengwa kusajiliwa wakati wa zoezi hilo kote nchini.